Ni saa chache kabla ya kufunga mwaka 2018, ndipo wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Mkoa waketi ili kujadili mustakabali wa masuala ya lishe ndani ya mkoa, kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita tarehe 31.12.2018
Akifungua kikao hicho, Mwl Shaban Kamchacho, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Geita na mwenyekiti wa kikao hicho,amewataka wajumbe kuwa huru kujadili wakitambua kuwa wao ndiyo wanaoiangalia lishe ya wananchi wa Geita huku akiwashukuru wajumbe wakiwemo wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuhudhuria kikao hicho muhimu.
Amesema, “kikao hiki ni muhimu kwakuwa bila lishe bora, hatuwezi kuwa na wazalishaji wa uchumi, wataugua na kutumia muda mwingi kujitibu, vilevile tukione kikao hiki kuwa ni cha manufaa kwa kutambua kuwa tunaangalia mustakabali wa lishe ya wanageita”.
Mwl. Kamchacho ameendelea kuwasihi wajumbe wa kikao hicho, kuhakikisha kila mmoja anakuwa sehemu ya kuihamasisha jamii kuzingatia lishe iliyobora ukizingatia kuwa Mkoa wa Geita unao wakulima, wavuvi, wafugaji n.k hivyo ni muhimu wakatambua kuwa si vyema kuuza mazao yote mfano maziwa na kuiacha familia bila chakula chenye lishe na kupelekea kudhohofu kwa afya zao.
Katika kikao hicho pia, imesisitizwa umuhimu wa Halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia tatizo la lishe kwa watoto wakiweka shilingi elfu moja kwa mwaka kwa kila mtoto itakayosaidia utekelezaji wa shughuli za lishe kwa lengo la kupunguza Udumavu kwamba jambo hilo ni la muhimu.
Katika taarifa yake, Bi. Tibezuka John ambaye ni Afisa Lishe Mkoa wa Geita amesema, bado jitihada zinahitajika katika kuongeza wataalam wa Lishe huku akiishukuru Serikali kupitia wadau Jhpiego-Boresha Afya kwa namna ilivyoratibu mafunzo ya IMAM (Integrated Management of Acute Malnutrition) kwa maafisa watano kutoka Mkoa wa Geita ya ambao kwa namna moja ama nyingine wataongeza nguvu kufuatia uhaba wa wataalam kwenye eneo hilo ili kuwasaidia watoto wenye UtapiaMlo.
Awali Bw. Frank Moshi kwaniaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa na Katibu wa Kikao chini ya mwongozo wa Mwenyekiti wa kikao aliwapitisha wajumbe kwenye muhtasari wa kikao kilichopita ambacho utekelezaji wake uliweza kutoa picha ya utekelezaji katika maazimio ya kikao kijacho.
Mwisho, wajumbe kwa pamoja walikubaliana kila mmoja kwenye eneo lake kuja na mkakati wa kuhakikisha suala la lishe linafanikiwa ndani ya mkoa watakapokutana kwenye kikao kijacho.
Miongoni mwa wajumbe wa kikao hicho ni baadhi ya wataalam wa Afya RHMT, Wakuu wa Idara, kutoka Sekretarieti ya Mkoa wakimo maafisa Ustawi wa Jamii, viongozi wa dini za kikristo na kiislam bila kusahau wadau Gelac na Neema House
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa