Na Boaz Mazigo- Geita
Kuelekea Miaka 59 ya Muungano Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Hamza Hassan Juma (Mb) amewataka wananchi kuupenda na kuuimarisha Muungano kwakuwa sisi ni taifa lenye nguvu kutokana na uwepo wa Muungano huo.
Ameyasema hayo Aprili 24, 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo la ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Geita iliyohudhuliwa na wananchi na viongozi mbalimbali na kupongeza jitihada zilizofanikisha ukamilishaji wa jengo hilo zuri na linalovutia.
“viongozi wetu hayati mwl.Julius Nyerere na Sheik Abeid Aman Karume waliona nchi zetu zimetawaliwa kwa muda mrefu na ili kuzuia chokochoko ambazo zingeweza kupenyezwa na wakoloni na wapinga maendeleo ili watu wasiishi kwa amani, tukapata muungano na kuwa na Taifa kubwa barani Afrika la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” alisema.
Mhe.Hamza aliongeza kuwa, “muungano huu siyo wa kubeza kwani hata wananchi waliungana hata kabla yake. Huu ni tofauti na mingine kwakuwa wengine walishindwa ila sisi baada ya kuungana tunaishi vizuri sana. Tuudumishe ili Tanzania yetu iendelee kuwa kisiwa cha amani. Mwisho nimpongeze Mkuu wa Mkoa Mhe.Martine Shigela kwa uchapakazi na niombe muendelee kumpa ushirikiano”.
Naye CP. Albert Nyamhanga aliyemwakilisha katibu mkuu Wizara ya mambo ya ndani alitoa shukran nyingi kwa Mkoa kufanikisha utendaji wa Wizara kwa kudumisha amani na usalama na kusema “huu ni miongoni mwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Wizara ya mambo ya ndani kupitia jeshi la Uhamiaji kwa mwaka wa fedha 2022/23 kati ya miradi ya zaidi ya bilioni 12”
Akitoa salamu za mkoa, Prof.Godius Kahyarara kwaniaba ya mkuu wa mkoa Geita alianza kwa kutuma salamu za muungano kwa viongozi wakuu wa kitaifa kuishukuru Serikali akisema “muungano wetu ni wa mfano, wenzetu walishindwa”. Vilevile alipongeza ujenzi wa jengo la Uhamiaji akisifu uzingatiaji wa thamani ya fedha. Aliongeza kuwa, Geita ni mkoa wa kimataifa na kwamba anaamini kwa uwepo wa ofisi hiyo utaendana na shughuli zinazofanywa Geita.
Awali akisoma taarifa ya mradi, kamishna wa fedha na utawala wa uhamiaji CIFA.Hamza Shabani alisema, “tunamshukuru sana Mhe.Rais.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio ya miaka miwili madarakani ikiwemo upatikanaji fedha za ujenzi wa majengo ya uhamiaji Geita na Linda ambapo kwa Geita jengo hili linagharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.5”. Kuhusu suala la ulinzi alisema ni la nchi nzima, hivyo kila mmoja analo jukumu hilo kwa kuwafichua waovu.
Kwa upande mwingine, Bw.Lucas Mazinzi kwaniaba ya CCM mkoa alianza kwa kuipongeza ofisi ya mkuu wa mkoa pamoja na kamati ya usalama kwa namna ambavyo imeendeleza umoja, upendo, mshikamano, amani na ushirikiano akisema, “sisi kama CCM tunashirikishwa kikamilifu”
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa