Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa ametoa pongezi kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Kampuni ya Plantcor Mining and Plant Hire (Pty) Ltd kutoka Nchini Afrika Kusini kwa kuingia makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa utafiti na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Kigosi, Wilayani Bukombe, Mkoani Geita.
Naibu Waziri wa Madini ametoa pongezi hizo tarehe 24 Februari 2026 alipokuwa akishuhudia hafla ya utiaji saini Mkataba wa Mashirikiano baina ya Shirika la Madini la Taifa na Kampuni hiyo ya utafiti na uchimbaji wa Dhahabu katika leseni ya Kigosi, shughuli iliyofanyika katika Mji mdogo wa Ushirombo Wilayani Bukombe.
Dkt. Kiruswa ametoa agizo kwa Menejimenti ya STAMICO kushirikiana kwa karibu na Plantcor ili kuhakikisha mradi unasimamiwa kwa weledi, uwazi na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa. Vilevile, amewataka wawekezaji hao kutimiza ahadi zote za uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia na kuzingatia Sheria za nchi ili mradi huo uwe mfano bora wa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi.
“ Baada ya kukamilika kwa utafiti wa kijiolojia, Plantcor itawasilisha taarifa za kina za maeneo yanayozunguka mradi wa Kigosi ili kuwawezesha wachimbaji wengine wenye leseni katika eneo hilo kunufaika na taarifa hizo kwa maendeleo ya shughuli zao. Hatua hii itafanya mageuzi makubwa katika uchimbaji Dhahabu kwa kutumia vipimo vya kiteknolojia.” Aliongeza Dkt. Kiruswa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigela amesema kuwa Mkoa wa Geita umejaliwa kuwa na hifadhi kubwa ya Madini ya Dhahabu na kutoa shukrani za dhati kwa Shirika la Plantcor kwa kuchagua kuja kuwekeza katika Mkoa wa Geita na kuahidi kushirikiana nao kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa Dkt. Venance Mwasse ameeleza kuwa faida zitakazopatikana kutokana na ushirikiano huo ni pamoja na kuzalisha na kuongeza ajira kwa watanzania, kukuza uchumi wa maeneo yote yanayozunguka eneo la Kigosi, kuongeza mapato ya Nchi na upatikanaji wa Teknolojia ya kisasa itakayoletwa na wawekezaji hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Plantcor, Joseph Wilmans ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya kuwakaribisha wawekezaji katika Nchi ya Tanzania na kubainisha kuwa kampuni yake imeleta utaalamu wa kiteknolojia na kifedha utakaosaidia kuongeza uzalishaji na ajira kwa Watanzania.
Ndg. Joseph Wilmans ameongeza kuwa Kampuni ya Plantcor ina uzoefu wa zaidi ya miongo miwili katika shughuli za madini kuanzia utafiti, uchimbaji, uchenjuaji hadi usambazaji wa bidhaa sokoni utakaowezesha sekta ya Madini kuzidi kukua kiuchumi.
Mkataba uliosainiwa unalenga kuvutia utafiti wa kina na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika uchimbaji wa Dhahabu ndani ya leseni saba zinazomilikiwa na STAMICO katika eneo la Kigosi. Pia STAMICO inaendelea kuwa lango la kuvutia mitaji na teknolojia za kisasa kwa manufaa ya Taifa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa