Katika kutekeleza kauli ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan isemayo, “Tunajenga Nchi Pamoja”, mkuu wa mkoa wa Geita Mhe.Rosemary Senyamule amekabidhi jumla ya mifuko 300 ya Saruji kwa taasisi za kidini, vyama vya siasa, pamoja na wananchi ili kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na wadau mbalimbali katika mnyororo wa maendeleo ndani ya mkoa, zoezi alilolifanya Mei 20, 2022 katika Bohari ya halmashauri ya wilaya ya Geita
Akikabishi mifuko hiyo, Mhe.Senyamule alisema, watu wa Geita ni wachapakazi na ndiyo maana aliguswa kuwaunga mkono akiamini kila mmoja kwa nafasi yake ana mchango mkubwa kwa maendeleo ya Geita na kusema pia unapounga mkono ujenzi wa misikiti na makanisa unaimarisha amani, umoja na mshikamano.
“kazi ya serikali ni kuongoza njia, kwakuwa watu wa Geita ni wachapa kazi niliona ni vyema niwaunge mkono pamoja na kuimarisha mahusiano mema na kuwatia moyo wananchi. Hivyo leo nakabidhi mifuko ya saruji 50 kwa Jimbo Kuu Katoliki Geita kwa ajili ya Kigango cha Magogo, 50 kwa ajili ya ofisi ya mtaa wa Lwenge, 50 kwa ajili ya Msikiti wa shilabela, 50 kwa ajili ya ofisi ya CCM Nyang’hwale na 100 kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba ya katibu CCM (M)” alisema Mhe.Senyamule.
Aliongeza kuwa, Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mengi mazuri na makubwa, hivyo kama wasaidizi wake nao wanaendelea kumuunga mkono na kumpa moyo katika ngazi za mikoa kasha kusisitiz juu ya wananchi kushiriki zoezi la anwazi za makazi, chanjo ya polio kwa watoto wa umri wa miaka 0-5 pamoja na sensa ya watu na makazi pale itakapoanza, lakini pia kuwaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa hamasa kwa waumini wao ili kufanikisha agenda hizo za kitaifa.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa mifuko ya saruji, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Geita Alhaj Said Kalidushi alisema, “mkuu wa mkoa, leo umefanya msingi bora kwa jamii. Umeonesha uadilifu mkubwa sana kwani umeahidi, umesema na kutenda, asante sana".
Kwa upande wao, Sheikh Tuwa Mohamed Tuwa wa Kata ya Kalangalala(BAKWATA), Padri Yohane Mabula wa Jimbo Kuu Katoliki Geita, na Diwani wa Kalangalala Mhe.Prudence Temba wamemshukuru mkuu wa mkoa kwa upendo na umoja aliounesha kwa kuunga mkono shughuli zao na kwamba mifuko hiyo itatumiwa kwa kazi stahiki na itasimamiwa vyema.
Geita ya Dhahabu, Utajiri na Heshima. Kazi Iendelee.
Inaendelea:
Boazi Mazigo
Ag.HGCU
Geita RS
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa