Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (Mb) amemaliza ziara yake ya kikazi Mkoani Geita iliyodumu kwa siku tatu akiwa amehaidi kuzifanyia kazi changamoto alizozipokea kutoka kwa uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita tarehe 28.07.2018.
Amesema, miongoni mwa masuala ambayo Wizara imejipanga kuyafanya katika kuboresha huduma za afya kwenye Hospitali za Rufaa za mikoa ni pamoja na kutengwa kwa bajeti ya Shilingi Bilioni Thelathini (30,000,000,000/=) ambazo zitawezesha hospitali hizo ikiwemo ya Mkoa wa Geita kuwa na kitengo cha dharura (emergency), chumba kizuri cha upasuaji (Theatre), jengo la mama na mtoto, ICU za watoto pamoja na watu wazima, bila kusahau watumishi wa kutosha ambapo hospitali ya rufaa ya mkoa imepewa jumla ya watumishi sabini (70) wakiwemo madaktari (16) na kusisitiza wapokelewe na wapewe ushirikiano kwa kuwa figisu figisu hazina nafasi kwa awamu hii.
Kwa upande wa huduma ya mionzi (X-Ray) amesema, “kwa sasa serikali ina mpango wa kuingia kwenye teknolojia mpya kwa kutumia utaratibu uitwao “Placement” yani tunaangalia mahitaji ya hospitali zetu kisha kutangaza zabuni ambapo vifaa vya kisasa vitafungwa sisi tutachangia huduma na endapo vifaa vitaharibika litakua jukumu la mzabuni kutengeneza. Sambamba na hilo, madaktari bingwa watakaa sehemu moja baada ya kuunganishwa mfumo ambapo mgonjwa atapigwa picha ya mionzi (x-ray) Geita, tafsiri inatoka mbali kupitia huo mfumo”.
Kuhusu dawa, Dkt. Ngudulile amewahakikishia watanzania kuwa, dawa zote muhimu mia moja sitini na saba (167) zipo hivyo hakuna changamoto isipokua ameagiza uandikaji wa dawa kwa majina ya kitaalam (Generic) mfano (paracetamol) na siyo ya kibiashara (Branded) mfano (Panadol, Sheladol, n.k ), jambo ambalo laweza msababisha mwananchi afikiri hakuna dawa fulani ilhali ipo hivyo kwa kufanya hivyo ni kuwakosea watanzania. Lakini pia akatumia muda huo kumtaka mganga mfawidhi Dkt. Brian Mawala kuhakikisha kuanzia jumatatu wiki ijayo orodha ya dawa zote zinarekodiwa na kupelekwa OPD na wodini.
Ametoa agizo kwa vituo vya kutolea huduma za afya kuhakikisha wanaandika muda sahihi/halisi anapopokelewa mgonjwa, anapokwenda maabara hadi wakati wa matibabu. Mfano saa 12:03, saa 01:16 na siyo kila mtoa huduma kuandika muda wa majumuisho mfano saa12 PM, saa 1 AM hii itasaidia hata kuangalia chanzo inapotokea tatizo.
Ameonya kuhusu kuacha utaratibu wa kutuma mialiko ya watumishi kwa majina badala yake, mialiko iandike kuomba mtumishi wa sifa fulani ili hiyo fursa ya mafunzo itumike kwa kuzingatia mahitaji ya hospitali kwakua uongozi ndio unajua nani anastahili kwenda mafunzo. Pia ameagiza kutumika utaratibu wa kubadili wanaokwenda mafunzo siyo kila siku mtu mmoja pekee na kuongeza kuwa mfumo uimarishwe kuasidia ukusanyaji wa mapato.
Amehaidi kuyafanyia kazi maombi kutoka hospitali hiyo yakiwemo madai ya watumishi, gari la kubebea wagonjwa (ambulance), ukamilishaji wa jengo la mama na mtoto ambalo lililopewa shilingi milioni ishirini (tshs.20, 000,000/=) na Mhe. Rais, pamoja na mchango wa mifuko mia moja ya saruji (100) kutoka kwa Mbunge wa Geita mjini Mhe. Constantine Kanyasu, na Mwenyekiti wa bodi aliyetoa milioni moja (tshs.1, 000,000/=) kwakuwa jengo lilipo ni dogo ukilinganisha na mahitaji.
Amekemea suala la watumishi wa afya kupigwa, na kusema “kama ikitokea mtumishi wa afya amekosea kuna taratibu zake na mamlaka za nidhamu, hivyo awe mwananchi au mtumishi mwingine haruhusiwi kumpiga mtumishi wa afya, hivyo kwa ambayo yalitokea uchunguzi unaendelea na wale wote watakaobainika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao”aliahidi.
Mbunge wa Jimbo la Geita, Mhe. Constantine Kanyasu, Diwani wa Kata ya Kalangalala mahali hospitali ilipo, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali na Mganga Mfawidhi kwa niaba ya watumishi na wananchi wamemshukuru sana kwa ujio wake Naibu Waziri na kuhaidi kupokea na kutekeleza maagizo aliyoyatoa, kisha naibu waziri kuendelea na safari yake.
Awali Naibu waziri alipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Eng. Robert Gabriel tarehe 26.07.2018 katika ofisi za Mkoa wa Geita
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa