Ikiwa zimebaki siku nane (8) kabla ya Jukwaa la Fursa za Biashara kurindima Mkoani Geita kuanzia tarehe 15-16.08.2018, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Mhandisi Robert Gabriel, ameendelea kufurahishwa na mwitikio mkubwa wa wawekezaji wanaopiga hodi ndani ya mkoa huu.
Amesema hayo alipompokea mwekezaji ndugu. Khalfan Abdullah Khalfan tarehe 07.08.2018 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ambapo mwekezaji huyo aliweza kueleza nia yake ndani ya mkoa huu.
Ndugu. Khalfan alisema, “nimetoka Dodoma jana, nimefika Geita, kwakweli nimeona zipo fursa nyingi za uwekezaji, hivyo mimi nitapenda kufungua kiwanda cha maji humu, maji yenye jina Geita,”. Hatua hii ni uungaji mkono wa juhudi za Mhe. Rais za kuifanya Tanzania ya uchumi wa viwanda.
Naye Mkuu wa Mkoa hakusita kuonesha furaha yake kwa mwekezaji huyo kwa kumpongeza kuichagua Geita kama sehemu sahihi ya kuwekeza, kisha kumwahidi ushirikiano kupitia wataalamu wa idara ya maji ili kuweza kufanikisha suala hili. “Haiwezekani umetoka Dodoma kuja kuwekeza Geita alafu ukwamishwe?, leo nenda na mtaalamu wetu ukaone na kutembelea vyanzo vya maji na baadaye taratibu zifuatwe ” aliongeza.
Kisha ndugu. Khalfan akatoa shukrani zake kwa mapokezi mazuri aliyoyapata na ushirikiano kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na kuahidi kuharakisha ujenzi wa kiwanda hicho kwakuwa tayari ameona ni fursa kubwa mno kwa yeye kuitumia ndani ya mkoa huu.
Mkuu wa Mkoa wa Geita bado anatumia fursa hii kuwakaribisha watanzania na wageni wenye nia njema kuja kuwekeza Mkoani Geita kwani mazingira ni salama na rafiki kwa uwekezaji, hautajuta kukanyaga ardhi ya Mkoa wa Geita kwa ajili ya uwekezaji, hapa ni mahali salama pa uwekezaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa