Katibu Tawala Mkoa wa Geita Denis Bandisa amemuomba Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye kuifanya Geita kuwa ya kwanza kwenye matumizi ya mpango wa anwani za makazi na Postikodi, huduma itakayomwezesha mwananchi kupata barua, mizigo au kifurushi atakachotumiwa akiwa kwenye makazi yake kutoka sehemu nyingine.
Ametoa ombi hilo Oktoba 2, 2019 mbele ya Naibu Waziri Nditiye baada ya kuwasili mkoani geita kwa ziara ya kikazi akiwa ameambatana na wataalam wa wizara anayoisimamia, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na wawakilishi wa Kampuni ya VODACOM huku akieleza baadhi ya changamoto za sekta ya mawasiliano kutokana na ukuaji wake ikiwemo ya matumizi mabaya ya mitandao.
Mhandisi Nditiye amesema, sekta ya mawasiliano inakuwa kwa kasi sana, na kwa mataifa mengine ndiyo hutegemewa kwa uinuaji wa uchumi na inahitajika sana na watu hivyo ni sekta mtambuka, jambo linaloifanya Wizara kwaniaba ya Serikali kuhakikisha inatoa kipaumbele kwenye sekta hii na kuifuatilia kwa karibu sana kisha kueleza lengo la ziara yake.
“lengo la kufanya ziara Geita kwanza ni kuangalia hali ya mawasiliano kwa ujumla, pamoja na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hii. Pili, kutokana na changamoto za mawasaliano, tumekuja kuelimisha juu ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole tukitambua kuwa, endapo ifikapo desemba 31, 2019 bado mtu hajasajili laini kwa alama za vidole, basi mawasilano kwake yatakoma, hatoweza kupokea simu na ujumbe wala kupokea mpaka pale atakapojisajili, hili litapunguza changamoto ya wizi wa mtandao. Mwisho, ni uhamasishaji wa mpango mkubwa wa anwani za makazi ili tuepuke mtu kwenda posta kufuata mzigo, barua au kifurushi bali kimkute nyumbani”, alisema Mhandisi Nditiye kisha kumkabidhi Katibu Tawala Mkoa vitabu vya Taarifa ya Utekelezaji wa Mradi wa Mawasiliano kuendelea na ziara yake kwenye wilaya ya Mbogwe.
Akiwa njiani kuelekea wilayani Mbogwe, Mhandisi Nditiye amekutana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel akiwa katika ukaguzi wa hatua za ujenzi katika mradi wa kuzalisha gesi itokanayo na taka za machinjio, mradi wa halmashauri ya mji geita unaotekelezwa kwa fedha za Benki ya dunia na kumweleza lengo la ziara yake kisha kundelea na ziara yake.
Imeelezwa kuwa, hadi sasa kata zote nchini zina postikodi na kwamba zoezi lililobaki ili kukamilisha hatua ya mwananchi kupokea mzigo akiwa kwenye makazi yake ni la kuzifikia halmashauri zote, kisha kutambua majina ya barabara na kuweka namba za nyumba ili sasa mwanachi aweze kufikiwa popote alipo kupitia utambuzi huo. Pia, zoezi hilo litarahisisha utendaji hata kwa jeshi la polisi kwa kujua ni wapi mwananchi Fulani anaishi, lakini vilevile itarahisisha kuwakamata waarifu kwakuwa tayari namba zao zitakuwa zimesajiliwa kwa alama za vidole.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa