Na Boazi Mazigo - Geita RS
Mkoa wa Geita umepokea Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 kutoka katika mkoa wa Shinyanga, mapokezi yaliyofanyika Agosti 2, 2023 katika kijiji cha Nyang’holongo, Halmashauri ya Wilaya Nyang’hwale ambapo mkoa unatarajia kukabidhi mbio hizo mkoani Kagera ifikapo Agosti 8, 2023.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru, mkuu wa mkoa Geita Mhe.Martine Shigela alisema, ukiwa mkoani Geita utapitia, kuona, kufungua, kuzindua na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi 59 yenye thamani ya Shs.29,209,364,945.
“niwakaribisheni wakimbiza mwenge wa Uhuru mkoani Geita, tumejiandaa na tutashirikiana kukamilisha zoezi hili. Aidha, niwapongeze wananchi wengi kwa kujitokeza kupokea mbio za mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu” alisema RC Shigela.
Baada ya makabidhiano baina ya mkoa wa Shinyanga na Geita, mwenge wa Uhuru ulikabidhiwa kwenye Wilaya ya Nyang’hwale na kuanza kukimbizwa ambapo umepita kwenye miradi 10 yenye thamani ya shs.2,026,984,658 ambayo yote imepitishwa.
Akiongea na wananchi katika maeneo mbalimbali ulipopita mwenge wa Uhuru, kiongozi wa mbio hizo kwa mwaka huu ndg.Abdalla Shaib Kaim amesisitiza uzalendo na usimamizi kwenye miradi ya maendeleo kwa kutambua fedha nyingi ambazo zimetolewa na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan. Pia, kiongozi huyo amehimiza juhudi za utunzaji mazingira kisha kushiriki kupanda miti.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zitaendelea Agosti 3, 2023 ambapo utapokelewa na Halmashauri ya mji Geita
Kaulimbiu ya mbio hizo mwaka huu ni “tunza mazingira, okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa