Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Mheshimiwa Sakina Mohamed ametoa rai kwa wazazi, walezi pamoja na wananchi wote katika Mkoa wa Geita kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanawawezesha watoto walioko shule kutimiza ndoto zao.
Mhe. Sakina Mohamed ametoa kauli hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita alipokuwa akiongea na wananchi waliohudhuria maadhimisho ya juma la Elimu ya watu wazima yaliyofanyika tarehe 05/09/2024 katika Uwanja wa Mwenge Uyovu, Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe.
Mhe. Sakina Mohamed amewaasa wanaume kuacha tabia ya kuwarubuni na kuwaharibia maisha mabinti walioko shule pamoja na kukemea vitendo vya mapenzi ya jinsia moja vilivyoshamiri katika jamii, kwa kufanya hivyo watakuwa wanawasaidia wanafunzi hao kutimiza malengo yao waliyojiwekea na kutimiza wajibu wa malezi ya watoto kikamilifu.
“Ndugu zangu wazazi na walezi nawasihi mshiriki katika kufuatilia maendeleo ya kitaaluma ya watoto, kuchangia chakula cha watoto wawapo shuleni, kuwalinda watoto wanapokwenda shule na kurejea nyumbani ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na mama Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye amejenga shule nyingi mpya na madarasa ya kutosha ili watoto waweze kupata fursa ya elimu.” Aliongeza Mhe. Sakina Mohamed.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Geita ametumia fursa hiyo kuziagiza halmashauri zote za Mkoa wa Geita kutenga bajeti inayotekelezeka ili kuwawezesha walimu wa elimu maalum kupata motisha kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata elimu na kuondokana na adui ujinga .
Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Geita Ndg. Cassian Luoga ametoa rai kwa wazazi na walezi wote kutowaficha majumbani au kuwahamishia vijijini mabinti waliopewa ujauzito wakiwa shuleni pamoja na wengine ambao walisitisha masomo kutokana na sababu mbalimbali bali wawapeleke kusoma kupitia mpango wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari ambapo Serikali ya awamu ya sita imetoa fursa kwa kundi hilo kurejea shule. Pia wazazi na walezi wametakiwa kutumia vyuo vya ufundi stadi vilivyoko katika Mkoa huo kuwapeleka watoto wakapate ujuzi wa aina mbalimbali.
Akisoma risala kwa niaba ya walimu wa Mkoa wa Geita, Mwl. Juliana Musika ametoa ombi kwa Serikali kugharamia na kuendesha zoezi la upimaji wa watu wazima wasiojua kusoma, kuhesabu na kuandika, Halmashauri zote kutenga bajeti toshelevu ili walimu wa elimu maalum waweze kutimiza wajibu wao kikamilifu pamoja na kutenga bajeti ya Elimu ya watu wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi ili kuondoa usumbufu usiohitajika.
Afisa Elimu Maalum Mkoa wa Geita Bi. Salome Cherehani ameeleza kuwa Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu wazima huadhimishwa kimataifa kila mwaka ikiwa na lengo la kujenga uelewa na kutambua changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya Elimu ya watu wazima katika jamii na kukumbusha watu juu ya umuhimu wa Elimu ya watu wazima. Maadhimisho ya mwaka 2024 yamebebwa na kauli mbiu isemayo “Ujumuishi katika Elimu bila Ukomo kwa Ujuzi, Ustahimilivu, Amani na Maendeleo.”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa