Geita umeendelea kuwa mkoa unaovutia uwekezaji huku ukiweka mazingira rafiki na wezeshi yasiyo na urasimu wala rushwa kwa wawekezaji wote wenye nia njema ya kuwekeza, jambo linalopelekea ugeni wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma PSSSF kupiga hodi Geita kwa lengo la kuwekeza kwenye ardhi na kupokelewa na mwenyeji Mhandisi Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Aprili 8, 2019 ofisini kwake.
Akizungumza na wajumbe wanaounda bodi hiyo, Mhandisi Gabriel amewaambia kuwa, Geita ni mkoa wa utajiri na wa kimkakati huku akiwaeleza jinsi unavyozalisha dhahabu kwa zaidi ya asilimia sabini, vilevile mkoa unaokwenda kufunguka katika sekta ya utalii kupitia Biharamulo, Burigi na Kimisi na kuwaibia siri ya mafanikio aliyoyapata na anayoendelea kuyapata katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile inayotumia fedha zinazotokana na mapato ya dhahabu.
“niwakaribishe sana kuwekeza mkoani hapa, hamtojutia. Nyumba za Kisasa za kupanga (apartment) na Hoteli ni miongoni mwa mahitaji makubwa kwa sasa mkoani hapa. Sisi kama serikali kazi yetu ni kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi ili mnapowekeza mpate faida, hakika mtaongeza imani kwa wateja wenu kwakuwa mtakuwa na hakika ya kuzalisha faida. Hatutaki kama mkoa kutegemea dhahabu pekee ndiyo sababu tunajipanga kukuza uchumi kwa kuweka miradi ya kimkakati, kuimarisha utalii kwani tumeamua na fedha ya kufanya hayo ipo”, alisema Mhandisi Gabriel.
Baada ya kumaliza mazungumzo ofisini kwake, Mhandisi Gabriel aliwapitisha wajumbe hao kujionea soko kuu la dhahabu geita ikiwa masoko mengine nane yataanzishwa hivi karibuni, akawaonesha uwekezaji unaotokana na mapato ya fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii (CSR) kutoka Mgodi wa Dhahabu Geita GGM huku akiwaambia , “sifanyi miujiza, nimezuia wezi kwenye miradi ndiyo maana nimefanikisha haya”.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Mussa Iyombe amemueleza mkuu huyo wa mkoa kuwa, wapo mkoani geita kuona eneo linalomilikiwa na PSSSF ili kujua ni kwa namna gani linawekezwa kisha kumshukuru mhandisi Gabriel kwa namna alivyowapokea na kuwakaribisha kuwekeza akiahidi kuyafanyia kazi mawazo waliyopewa akisema, “tumefurahia mawazo yako, tuna ahidi kuwa karibu nawe katika kufanikisha miradi tutakayoitekeleza Geita”
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa