Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe imetajwa miongoni mwa halmashauri za mkoa wa geita zilizopata hati inayoridhisha “Unqualified Opinion” kupitia taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali CAG ya mwaka wa fedha 2017/2018, taarifa iliyosomwa julai 18, 2019 kwenye Mkutano wa Baraza Maalum Kujadili Hoja za CAG katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Bukombe.
Akiahirisha mkutano huo, mwenyekiti ambaye ni Mkuu wa Geita mhandisi Robert Gabriel ameipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati inayoridhisha huku akitoa muda wa kuhakikisha majibu ya hoja zote zilizosalia yanapatikana ili kufuta hoja hizo.
Amesema, “ili halmashauri iendelee, ni lazima tuhakikishe hoja zoye zinajibiwa, hivyo nawapa wiki 2 mhakikishe majibu ya hoja zilizosalia yanapatikana. Vilevile ongezeni mapato hata kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato na mhakikishe vikao vyote vya kisheria vinaketi na mdumishe uwazi, fedha yoyote inayoingia ni vyema madiwani wakaelewa vilevile wakajua na utaratibu wake”.
Mhandisi Gabriel amewaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa, umoja ni ushindi na kwamba watambuwe kuwa, wote ni timu moja ya ushindi wa Mhe.Rais Magufuli kisha kuahidi kuleta mradi wa upimaji viwanja wenye thamani ya shilingi Milinoni 100
Mustafa Saidi kwaniaba ya Mkaguzi Mkuu wa Nje amesema, bado utekelezaji wa maoni ya CAG kwa halmashauri ya bukombe siyo wa kuridhisha kwani kati ya hoja 76, zilizotolewa kwa hesabu za 2017/2018 zikijumuisha hoja za miaka ya nyuma, ni hoja 41 tu zimepatiwa majibu ya kuridhisha na kufungwa na hivyo hoja 35 sawa na 46% zinaendelea kusalia.
Ushauri kutoka sekretarieti ya mkoa ukawa ni halmashauri kuhakikisha wanajibu hoja kwa wakati kwakuwa muda huwa ni mwingi unaotolewa wa maandalizi kabla ya kazi kuanza lakini pia kupitia sheria ndogo na kuzifanyia marekebisho ziendane na wakati huu kutokana na mabadiliko ya masuala mbalimbali ya ushuru na kodi kubadilika bila kusahau kuwa na mpango kazi wa ulipaji wa madeni.
Mkuu wa Wilaya hiyo Said Nkumba na Mwenyekiti wa Halmashauri Safari Mayala kwaniaba ya Halmashauri ya Bukombe wakamuahidi mkuu wa mkoa kufuata maelekezo yote yaliyotolewa na kwamba watahakikisha hoja hizo zinajibiwa kwa wakati ili waendelee kupata hati inayoridhisha.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na mbunge wa jimbo la bukombe ambaye pia ni waziri wa madini Doto Biteko akiwa miongoni mwa viongozi wanaohudhuria mikutano mbalimbali jimboni kwake.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita
Sanduku la Barua: S.L.P 315
Simu: 028 2520035
Mobile: 028 2520035
barua pepe: ras.geita@tamisemi.go.tz
Hakimiliki©2017Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Geita. Haki zote zimehifadhiwa